ASKOFU KINYAIYA AWAASA WAAMINI KUMUOMBA MUNGU WANAPOKUMBANA NA CHANGAMOTO KATIKA MAISHA,AWATAKA KUTOKUWA KIKWAZO KWA WATU WENGINE.

Askofu Mkuu wa Jimmbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya, amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutochoka kusali na kumuomba Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwapa majibu ya  changamoto wanazozipitia katika maisha yao.

Amesema hayo wakati wakati akitoa homilia yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya sakramenti ya Kumunyo ya kwanza kwa vijna 40 na kuwaimarisha kwa mapaji 7 ya Roho Mtakatifu Vijana 24,katika Parokia ya Bikira Maria Immakulata-Chamwino.

“Wote tunapitia changamoto za maisha ambapo zipo nyingi tu, wengine kuwa wagonjwa na kama sio wewe basi ndugu yako, jamaa au rafiki yako katika familia wengine tuna changamoto za uchumi unayumba,wengine tunachangamoto za mahusiano mume na mke maelewano ni shida kidogo, wengine ndugu kwa ndugu katika familia wengine majirani.

 

Changamoto za kila aina kama hazijakupata basi tambua kwamba zitakufikia tu wakati flani, kuna wazazi wanahangaika sana wamejaribu kuwalea vijana wao kwa uwezo wao wote na hata kuwapeleka katika shule wakawasomesha wakawashauri wakafanya kila walichoweza kufanya ili hawa watoto waweze kuwa watu safi.

Lakini matokeo yake baadhi ya hao watoto ambao wamehangaikiwa hivyo na wazazi wamekuwa wapowapo tu,kazi hawataki kufanya kanisani hawaendi kusali hawasali wazazi wanahangaika na kufikia wakati wanajiuliza Mwenyezi Mungu kimetokea nini?” amesema Askofu Kinyaiya.

Aidha amesema kwa namna ya pekee kama Taifa,waamini waendelee kuomba ili Mwenyezi Mungu aondoe balaa la ugonjwa wa UVIKO-19 kwani bado ni changamoto katika Taifa na ulimwengu mzima, huku akiwataka kuendelea kuchukua tahadhari na kusikiliza maelekezo ya wataalamu wa afya.

Katika hatua nyingine Askofu Mkuu Kinyaiya amesema kuwa, yeyote anayefanya jambo jema la Kimungu hata kama si wa kundi la jamii fulani au kiimani, kamwe asitokee mtu wa kumzuia au kumpinga.

Amesema kwamba Mwenyezi Mungu ana njia zake mbalimbali za kufanya kazi na kusaidia watu wake ndani na nje ya Kanisa, hivyo asitokee mtu wa kupinga pale anapotokea mtu anayefanya jambo  jema la Kimungu na badala yake mtu huyo ashauriwe aendelee kufanya vizuri zaidi.

“Tunaambiwa tusiwe kikwazo au kizuizi katika maisha ya kwa ajili ya watu wengine kwasababu adhabu yake ni kubwa ni kufungiwa jiwe kwahio niombe kila mmoja wetu afikirie kwamba umeshawahi kufanya lolote ambalo likawa kizuizi kwa mwingine,likamfanya mwingine akaanguka iwe kiroho au kimwili,na kama ni hivyo tunaambiwa tuombe msamaha,” amesema.

 

Hata hivyo Askofu Mkuu Kinyaiya amewaomba waamini kuepuka tabia ya kuwakwaza watu wengine kwa makusudi na kuwasababishia hali ya kuanguka dhambini.

Amesema hata katika maisha ya jamii wapo baadhi ya watu wamekuwa kikwazo cha mafanikio ya wengine kwa namna mbalimbali,hivyo amewaonya waamini kujitafakari kwa kina na kuacha kuwa kikwazo kwa wengine.

“Kama wewe upo katika nafasi ya kumsaidia mwenzako kupata cheo kazini na unaulizwa utoe ushauri kwamba huyu vipi tumpandishe cheo au la,lakini wewe kwasababu ya roho yako ya korosho unasema huyu hafai kabisa kabisa,wewe ni kikwazo kwa mwenzako na unaambiwa adhabu yake ni kufungiwa jiwe shingoni.

Kwahio wale wote wenye roho ya korosho tunaonywa badala yake tupende kusaidiana katika maisha tusiwe kikwazo kwa wenzetu, au wewe ni bosi mahali ni mkubwa kimadaraka katika sehemu uliyopo lakini waliochini yako unawanyanyasa mapaka wanajisikia kwamba wao ni wadogo sana,wanajisikia hawana maana kwa jinsi unavyowatenda,hicho ni kikwazo na wewe ni kikwazo kwao hivyo tunaonywa tujitazame upya wapendwa tafadhali.

 

Au pale unapomkatisha mtu tamaa anakuja mtu amekuona umefanikiwa katika jambo fulani labda ameona unafanya biashara nzuri anakuja kuomba ushauri hebu ndugu yangu naomba unishauri namimi nifanye biashara nzuri kama wewe.

halafu unamwambie wewe achana na hiyo huwezi kabisa utakula tu mtaji acha hiyo biashara huwezi, unamkatisha tamaa jumla asifanye lile jambo alilotaka kulifanya wewe ni kikwazo,” amesisitiza Askofu Kinyaiya.

Akizungumza na Vijana waliomarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara na waliopokea kumunio ya kwanza,amewataka kuendelea kumuishi Roho Mtakatifu waliempokea kwa kushiriki masakramenti mbalimbali za kanisa na kuwa watu wa sala.

Pichani, ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap, akiwa katika Picha ya pamoja na baadhi ya Vijana waliomarishwa kwa sakramenti ya Kipaimara na waliopokea kumunio ya kwanza,mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria Immakulata-Chamwino, kushoto kwa Askofu ni Paroko wa Parokia hiyo ya Chamwino Padre Paul Mapalala.